Wednesday, October 26, 2016

KUWEKA NA KUTIMIZA MALENGO

Usikubali ngono ikatishe maisha yako. Weka malengo, timiza ndoto zako na UCE

KUWEKA NA KUTIMIZA MALENGO
Utangulizi
Kila mtu duniani hutumia muda mwingi kutafakari kuhusu maisha yake ya sasa na baadaye. Isitoshe kila mtu anatamani kubadili mojawapo ya jambo katika maisha yake. Yawe maisha ya kifamilia, marafiki, uhusiano au kipato. Inawezekana kubadili jambo. Hatua ya kwanza ni kuweka malengo juu ya hilo jambo.

Kuweka malengo ni utaratibu rasmi wa mipango unaozingatia kuchagua, na kupanga hatua kwa hatua katika kufanikisha jambo. Lengo la somo hili ni kutoa elimu juu ya kuweka na kutimiza malengo yako (sehemu ya I) katika maisha kwa ajili ya kuwa na:
  • Maisha yenye afya
  • Mahusiano yenye afya
  • Kazi na wajibu

Faida za kuweka malengo
  1. Kufanikiwa zaidi katika maisha
  2. Kuboresha mafanikio kiujumla
  3. Kuongeza motisha ya kufanikiwa zaidi katika maisha
  4. Kuongeza fahari na furaha katika mafanikio yako
  5. Kuongeza kujiamini na kukua kwa utu wa mtu
  6. Kuondoa mtazamo unaokurudisha nyuma na kukusababishia kukosa furaha
  7. Kupungua kwa msongo na hali ya wasiwasi uliopindukia zaidi

Kuweka malengo ni njia iliyowafanikisha wafanyabiashara wengi, wanamichezo (wakimbiaji) na kadhalika. Kuona mafanikio ya malengo yako hukuza kujiamini zaidi na kujenga imani ya uhitaji wa kutimiza malengo ya juu zaidi na magumu.

Kuchagua lengo sahihi la kuanza nalo wakati mwingine ni vigumu. Lengo huanzia na jambo unalotaka kufanikisha na unataka kuyaendeshaje maisha yako. Hili ni la msingi kwani lengo hutoa dira ya muda mrefu, na motisha wa muda mfupi. Humsaidia mtu kutoa kipaombele na ujuzi unaomsaidia kupangilia rasilimali alizonazo. Unaona mbali katika lile lililoonekana awali kuwa jitihada zisizokuwa na maana.

Malengo huwekwa kwa madaraja mbalimbali. Maswali ya kujiuliza ni:
  1. Unataka kufanya nini na maisha yako?
  2. Unataka kufanikisha nini?
Baada ya kujibu maswali hayo, unayavunja katika makusudio madogo madogo yatakayokusaidia kutimiza malengo ya maisha. Kisha uyafanyie kazi.

UCE team haifungwi na umbali, iwe mlimani, bondeni porini, tutakufikia kukuelimisha. Pichani ni Afisa uhamasishaji wa UCE Mr Mgina akitoa semina kwa wanafunzi wa Wasa Sekondari



Madaraja ya Kuweka Malengo
  1. Afya:   Je unataka kuwa na afya ya aina gani kimwili, kiakili, kijamii na kiroho?
  2. Mtazamo: Upi mtazamo wako wa kimaisha?
  3. Kipaji / karama: Je una kipaji gani?
  4. Elimu / Ujuzi: Je ungependa kujiajiri au kuajiriwa?
  5. Familia: Je ungependa kuwa mzazi wa aina gani?
  6. Fedha: Je ungependa kuwa na kipato cha aina gani? Katika umri gani?
  7. Starehe: Ungependa kuyafuraiaje maisha yako?

Kupanga na Kuweka Malengo
Je ni mara ngapi umefanya uamuzi juu ya kisababishi cha jambo na hukuweza kulifuatilia? Isitoshe tatizo la wengi wetu tumekuwa tukiweka malengo yale yale kila siku na kila mwaka ambapo hatukuwai kufanikiwa. Isitoshe kama tumefanikiwa kwa nini kuendeleaza hayohayo tu kila mwaka?

Jifunze kuweka malengo ya miezi sita, mwaka, miaka mitano, au miaka kumi. Malengo yako yawe yenye kuleta mafanikio, unayoyafurahia, yenye kuzingatia tarehe, muda na kiasi / kiwango ili kuweza kupima mafanikio ya malengo yako. Zingatia kutoa kipaombele katika kuchagua lengo la kuanza nalo, yaandike malengo yako, hatua uzipitiazo na yale uyafanyayo katika kutimiza malengo yako. Yaweke malengo yako katika mambo madogo madogo utakayoweza kuyatimiza na kuyamudu. Kumbuka ili uweze ktutimiza malengo yako kuwa na nidhamu ni jambo la msingi.

Unapofanikisha lengo pata muda wa kujipongeza. Kutokana na ulilotimiza panga lengo lingine gumu kidogo ya lile ulilofanikisha. Iwapo kuna funzo ulilojifunza kutokana na lengo ulilofanikisha na unaona umuhimu wa kubadili jambo kwa malengo yajayo fanya hivyo. Kama unahisi kukosa ujuzi katika malengo panga lengo la kutatua hilo mf. Ongeza lengo la kupata ujuzi. Kumbuka malengo ni mtumwa wako na sio bosi wako.

Mratibu Mipango UCE Mr Lema , katika semina Ilula , ukanda wa Mazombe


Mfando wa Jedwali la Kupanga Malengo
Aina / Eneo la Lengo m.f. Afya n.k
Faida za Lengo Husika
Mchakato / Ufunguo
Muda
Rasilimali
Matokeo
Toa maana ya lengo lako, liandike kutokana na mpangilio na kipaombele
Orodhesha faida utakazopata kwa kufanikisha lengo lako,

Jambo gani litakufanya uwe mwenye furaha?
Hatua zipi unatakiwa kufuata ili kutimiza lengo lako,


Je utaanza na hatua ipi?
Andika muda wa kuanza na utakaohitajika katika kulitimiza lengo lako
Andika mahitaji yanayohitaji-ka katika kulitimiza lengo

Je utazipata wapi?
Umefanikisha nini? 
Wapi umekwama, na zipi sababu za kufanikiwa au kukwama?
Je lengo lako litaleta athari gani katika maisha ya sasa na yajayo?

Kupanga Malengo Kunapofanyika Kimakosa
  1. Kupanga malengo ya matokeo pasipo kupangilia utekelezaji wake hatua kwa hatua
  2. Kupanga malengo yasiyo na uhalisia kwani hakuna jitihada za kuyatimiza
  3. Kupanga malengo yasiyoleta changamoto wala faida inayoonekana
  4. Kutokuwa na mpangilio wa lipi lianze na lipi lifuate
  5. Kupanga malengo mengi kwa wakati mmoja

Kicheko cha kiwango cha lami kwa mwanafunzi wa Nanenane sekondari Morogoro baada ya kufanya maamuzi ya kusubiri kwa kusaini kadi ya UCE.


Zingatio
  1. Tafakari na jenga taswira ya maleongo yako
  2. Fikiria yapi yanaweza kukwamisha malengo yako
  3. Ainisha na bainisha mambo yatakayokusaidia kutimiza malengo yako
  4. Pitia mara kwa mara malengo yako
  5. Jiwekee yapi ya kufanya na yasiyo ya kufanya (Do’s and Don’ts)
  6. Jifunze kutawala muda wako vizuri (time management) kwa kuoorodhesha yale yanayoiba au kupoteza muda wako
  7. Jifunze kutawala msongo katika hatua zote za malengo yako
  8. Usiweke malengo madogo kwa kuhofia kushindwa
  9. Ni vyema kujua kushindwa kutimiza lengo haijalishi sana iwapo kuna funzo umejifunza katika hilo lengo
  10. Kumbuka malengo yako yawe kwa yale unayotaka kufanikisha katika maisha yako kwani mafanikio huja pale unapofanya kwa ajili ya ustawi wako
Wanafunzi wa Mbalali sekondari mkoani Mbeya wakifurahia maamuzi yao ya kusubiri. INAWEZEKANA

Karibu UCE Taanzania ujifunze mengi  juu ya kulinda na kuimarisha afya



Mtayarishaji / Mwezeshaji
Kazi hii imetayarishwa na kufundishwa Mr. Isaac S. Lema Mratibu Mipango UCE Tanzania
Kitaaluma: Mshauri (Professional Counsellor) Shahada ya ushauri toka chuo kikuu cha Tumaini Iringa
Tabibu Msaikolojia (Clinical Psychologist) shahada ya uzamili toka chuo kikuu cha Muhimbili Dar es Salaam;
Mawasiliano: Namba ya Simu: 0713 778808, 0764 345 318 Barua Pepe: lemaisaac@yahoo.com


Posted by Eng Nguki Herman. UCE Morogoo Regional Coordinator.
O763639101/ ngukiherman@ymail.com
www.ucetanzania.org
Share:

Monday, October 24, 2016

KWANI KUNA TATIZO?


KWANI KUNA TATIZO?
Kama nakusikia vile, karibu bhana tuwe wawili nje huku.

Katika mizunguko yangu ya siku zote, huyooooooo hadi hospitali ya  mkoa wa Njombe maarufu kama Kibena. Wakati nimekaa nje ya hospitali kando ya barabara nikamuona mama mmoja (sio mkubwa sana, ni binti kijana) ambaye alikuwa mjamzito. Alikaa chini kabisa kwenye nyasi huku akiwa mpole na akionekna kutafkari na mwenye mawazo mengi sana. Kiufupi ilionekana kuna kitu kinamuumiza kichwani kwake, au anamaumivu ya mwili, si unajua tena hawa ndugu zetu wakiwa katika hali hiyo complications kibao.
Baada ya muda mfupi watu wakatokea hospitalini kuja upande wa barabarani. Ni kijana mmoja na binti mmoja ambaye alikuwa mjamzito pia. Bila shaka walikuwa mtu na mkewe kwa maana niliona Yule mkaka kamshikia mkoba huyu dada, pia kamshika mkono huku wakiwa wanatazamana usoni kwa bashasha na matabasamu ya kukata na shoka. Kha, nikajua ni mimi tu ndio nilikuwa nawangalia wale watu kama sehemu ya tuition, kumbe hata yule dada aliyekaa kinyonge pale chini alikuwa anawakodolea macho vizuri tu. Muonekano wa wawili hawa ulitoa picha ya moja kwa moja kuwa wanaishi maisha ya furaha na walijipanga vya kutosha, tena hawajutii maamuzi yao na matokeo yake. Yule dada pale chini liendelea kuwaangalia kwa uchungu huku machozi yakimlengalenga (sina hakika kama ni Kiswahili sahihi), aliwangalia hadi walipovuka barabara na kuendelea kuwasindikiza kwa macho hadi walipoingia kwenye gari la kuelekea Njombe mjini. Kisha akajiinamia chini huku ameshika shavu lake.
Mimi kama kijana nilijiuliza maswali mengi mepesimepesi na kujijibu mwenyewe. Kwa mfano huyu mama hapa chini tena akiwa kachafuka na vumbi huenda kaolewa lakini mumewe hajuwi majukumu yake kwa matokeo ya kile ambacho alikifanya yeye mwenyewe. Au yamkini akawa hii mimba kapewa na mtu ambaye hajamuoa bado hivyo mhusika kakataa kushughulikia lolote nakadhalika, au pengine jamii nzima inayomzunguka imemtenga kwa mfumo fulani.
Ndugu zangu mama mjamzito mwenye msongo wa mawazo  sio tu huathiri mfumo wa kawaida wa maisha yake, lakini pia huathiri afya ya mtoto tumboni nap engine kumzaa motto mwenye afya mbovu ya mwili au akili au vyote kwa pamoja. Mvulana ukikurupuka kwa kuendeshwa na hashiki za mwili kasha kumdandia kwa pupa huyo uliyemshawishi kwa pesa zako, unatengeneza bomu ambalo litakulpukia hapahapa duniani au hata ile siku utakaporudi kwa yule aliyekuleta duniani.

Mfano hebu fikiria mama mjamzito ambaye kaolewa na yuko na mumewe nymbani halafu usiku tumbo limuume kidogo, utasikia:
Mama : We baba kijacho, amka bhana mwanao kanipiga teke tumboni hapa, linauma.
Baba   : Oh, pole my love, kwahiyo ngoja nimpigie rafiki yangu aje na tax twende hospitali.
Mama   : Hapana acha tu usiku sahizi, nitajitahidi kuvuilia tutaenda hata asubuhi.
Baba     : Hapana, plz, au tumpigie simu Dakitari aje akucheck hapahapa nyumbani.
Mama   : Mhhh, usiku wote huu, usijisumbue, acha tu mume wangu.
Baba     : Haya mama, basi ngoja tukae wote, silali hadi muanze  kulala wewe na kijacho wangu.
Mama   : Hahaaa, acha bhana, unadhani tumbo lenyewe linauma sana basi, nilitaka tu uamke nikusikie kidogo baba kijacho waangu.
Baba    : Duh, jamani haya mama. Minahamu na huyo kijcho kama nini, sijui katakuwa kajogoo,au ndio mama ndio atajipatia mke mwenza,, teh, heh, (anacheka huku akimbusu tumboni mkewe). Akizaliwa nitamwambia ulimsingizia kuwa kakupiga teke kwa ndani kumbe ulitaka kusikia tu sauti ya baba yake. Haya mama, lala basi nikufunike shuka                            … …………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………………
Umeona haya majadiliano? YANA AFYA, RAHA nakadharika.

Hebu tuwe wakweli. Dada ambaye kapewa mimba na mtu ambaye hajamuoa bado. Hapo nyumbani wamemdongoa hadi basi, wamemsondea dole hadi basi, (hadi huyo motto anajiuliza kwani huko nje kuna vita?) tumbo likiuma usiku anamuamsha nani? HAKUNA KITU ZAIDI YA KUJIONA MKOSAJI NA KUMCHUKIA MTOTO ANGALI YUKO TUMBONI. Kwa bahati mbaya mtu ambaye hayajamkuta, anaona ni kitu cha kufikirika nay eye hakiwezi kumkuta wakati hataki kubadilika. Huo ni mtazamo wa mtu mjinga. Maana mwerevu hujifunza kupitia matatizo ya watu wengine, lakini mjinga haamini hadi yamkute yeye, ili werevu wajifunzie kwake kama sample space.
Badilika na uchukue hatua leo, kama ulishakosea basi usirudie tena, na kama Mungu amekuepusha hadi sasa, basi usifanye makosa kwenye kufanya maamuzi. Fanya uchaguzi sahihi, funga ndoa halali, furahia wakati wa ujauzito wako/ wa mkeo kwa raha zenu. Inawezekana…
 Kwa kijana ambaye una malengo mwngiiiiii, itumie UCE Tanzania ikusaidie kuweka mikakati thabiti ya maisha yako n kamwe huwezi kujutia. USIFANYA NGONO KABLA NA NJE YA NDOA. TRUE LOVE WAITS………….Tafakari njema

Ukisikia UCE wanaongea na wanafunzi au wtu fulani, fanya hima uwepo ili kujichotea maarifa ya kuishi maisha yenye afya.

Maelfu ya vijana mwameshafikiwa na team ya UCE hata kwako twaweza kufika. Karibu tujifunze pamoja,


Eng Herman Nguki
UCE Tanzania Volunteer
+255 763 639 101/+255 679 639 101 /ngukiherman@ymail.com

Ngukiherman.blogspot.com / ucetanzania.org /uceglobal.org
Share:
Designed and Developed by Joel Elphas +255 757 755 228 E-mail: elphasjoel@yahoo.com © UNIVERSAL CHASTITY EDUCATION (UCE) -TANZANIA ...Helping people live healthy lives. | ronangelo | NewBloggerThemes.com